NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, ameelezea kukerwa na
siasa za majungu na vikao vinavyoishia kupigana ndani ya chama chake na
badala yake amewataka viongozi wenzake kuelekeza nguvu kwa wanachama,
kwani malumbano hayatakijenga chama.
Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, alitoa kauli hiyo jana, baada ya RAI Jumatano kutaka kujua
msimamo wake kutokana na kuhusishwa kuwa nyuma ya usaliti anaodaiwa
kuufanya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Katika majibu yake hayo aliyoyatoa
kwa njia ya mtandao, Zitto alisema wanaojaribu kumhusisha na suala la
Mwigamba ni kawaida yao kupenda kumhusisha na mambo yasiyomhusu.
“Mwigamba ni Mwenyekiti wa chama wa
Mkoa mwenye utashi wake wa kisiasa. Ana uwezo wa kusimama mwenyewe. Siyo
kila mtu mwenye mawazo yake anatumika. Sasa hao wanaomtuhumu Mwigamba
wao wanatumiwa na nani?” alihoji Zitto.
Kuhusu hoja kwamba sakata hilo la
Mwigamba chanzo chake ni msuguano wa kuwania nafasi ya uenyekiti kati
yake na Mbowe, Zitto alisema uchaguzi ndani ya chama haujatangazwa, kwa
hiyo yeyote anayezungumzia kugombea au la anavunja kanuni za uchaguzi.
Katika hilo, Zitto alisema hahitaji mtu wa kumsemea, kwamba akihitaji uenyekiti wa chama atasema yeye mwenyewe.
“Nina sifa zote, siyo tu za kuongoza
chama, bali kuongoza nchi. Nina elimu ya kutosha, nina rekodi ya kazi za
kibunge kubwa kuliko wabunge takribani wote wa sasa, kwa miswada
binafsi, hoja binafsi na hata kuibua masuala nyeti ya nchi.
“Uadilifu wangu hauna shaka, uzalendo
wangu kwa nchi yangu ni wa kupigiwa mfano. Zaidi ya yote, najua kero za
wananchi na changamoto zao. Sihitaji kusemewa na mtu. Nikitaka
uenyekiti nitasimama mwenyewe,” alisema Zitto.
Zitto alisema kitendo cha kutaka
kumhusisha na masuala yanayoendelea ndani ya Chadema na kuhusu sakata
zima la Mwigamba, ni kutaka kuhamisha mjadala na kumtoa kwenye ajenda ya
kuwafuatilia watu wanaodaiwa kuficha mamilioni ya fedha nje ya nchi.
“Kwa sasa nina kazi ya kuhakikisha
mafisadi na wahuni ‘criminals’ walioficha fedha na mali nje ya nchi
wanaibuliwa na kurejesha fedha hizo,” alisisitiza Zitto.
Kuhusu madai ya kuchunguzwa na chama
chake kama na yeye ni mmoja wa wasaliti, Zitto alisema kuwa hizo ni
mbinu za kumuondoa kwenye kazi anayofanya ya kupambana na ufisadi.
“Wanajua nikishika jambo siachi mpaka
mwisho, hivyo wanajaribu kutengeneza uongo wanaouita uchunguzi.
Watanzania wasipumbazwe na vituko vya siasa vinavyoendelea. Tuendelee
kudai Katiba Mpya na kupambana na ufisadi. Kwa Wanachadema tuendelee
kujenga chama kwenye kanda zetu. Chama kitakachochukua dola ni kile
chenye mtandao mpana kwenda vijijini,” alisema.
Zitto aliwataka viongozi wenzake na
wanachama wa Chadema kupunguza vikao vya majungu vinavyoishia kupigana
na badala yake waende kwa wananchi wakafanye kazi, kwamba malumbano
hayajengi chama.
Kwa upande mwingine, chama hicho
kimeendelea kusisitiza kuwa madai yote yaliyotolewa na Mwigamba dhidi ya
chama chao ni ya upotoshaji, uongo na ya kichonganishi.
Kwa mujibu wa tarifa iliyotolewa kwa
vyombo vya habari na Ofisa Habari Mwandamizi wa chama hicho, Tumaini
Makene, wameshangazwa na hatua ya Mwigamba kuendelea kuvunja katiba ya
chama kwa kutunga mambo yasiyokuwepo, badala ya kuwasilisha hoja zake
kupitia vikao halali vya chama.
Alisema kwa kuwa Mwigamba amekiri
mbele ya waandishi wa habari kuwa amevunja katiba ya chama na kukubali
kuwa aliandika kwa kutumia jina bandia waraka na kuuweka kwenye mitandao
ya kijamii, ni wazi hana lengo zuri na chama chao, hivyo apuuzwe
MTANZANIA