Friday, October 4, 2013

TUTAISHAMBULIA TENA KENYA KUUA WATU ZAIDI, MITO YAO ITATIRIRISHA DAMU"......AL-SHABAAB


KIKUNDI cha Al Shabaab kimetishia kumwaga damu zaidi Kenya kwa kufanya mashambulizi mapya na safari hii wanatamba kupiga patakapouma zaidi. Kundi hilo limesema kwamba litaongeza idadi ya watu katika kikosi cha mashambuzi nchini humo kutokana na Kenya kukaidi kuondoa majeshi yake Somalia.

Msemaji wa AL-shabaab

Tutaishambulia Kenya sehemu itakayowauma zaidi, tutageuza miji yao makaburi na mito ya damu itatiririka Nairobi nzima,” al Shabaab ilisema katika taarifa yake na kuongeza:
Uamuzi wa Serikali ya Kenya kuendelea kuyaacha majeshi yake Somalia ni ishara ya wazi kwamba, hawajataka kujifunza kutokana na yaliyotokea katika shambulizi la Westgate,” ilieleza taarifa hiyo huku ikijigamba kuwa, Kenya itakuwa eneo litakalogubikwa na wingu la damu na vurugu.
Wakati kikundi hicho kikitoa tishio hilo, takriban miili isiyopungua tisa imepatikana katika eneo la ndani ya kifusi kwenye jengo hilo, na sehemu ya eneo liliunguzwa kwa moto wakati wa shambulio hilo la Westgate.
“Baadhi ya miili haiwezi kutambuliwa kabisa na utambuzi wa vinasaba (DNA) utafanywa ili kutambua, mingine imeharibiwa na inatisha,” taarifa kutoka Polisi ilieleza.
Hata hivyo haikuwekwa wazi kama idadi ya miili hiyo tisa imejumlishwa na watu 67 wakiwemo wanajeshi sita waliokufa katika shambulizi hilo. Rais Kenyatta ajibu Hata hivyo Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, juzi alikaririwa akisema majeshi yake yataendelea kubaki Somalia hadi hapo amani na usalama wa nchi nchi hiyo vitakapotengamaa.
Septemba 21 Shambulio la Westgate lililotokea Septemba 21 mwaka huu katika jengo hilo la maduka ya bidhaa mbalimbali za watu wenye maisha ya juu, wanadiplomasia na wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya Kenya.
Mbali ya vifo hivyo vilivyofahamika hadi sasa, watu zaidi ya 170 walijeruhiwa vibaya huku wengine wakipata matatizo ya kisaikolojia. Miongoni mwa waliouawa ni watoto waliokuwa kwenye tamasha la mashindano ya kupika kwenye jengo hilo.
Baadhi ya manusura wa shambulio hilo walieleza namna walivyokutana uso kwa uso na magaidi hao. Kupitia taarifa mbalimbali, magaidi hao walisikika wakidai wanawasaka Wakenya na Wamarekani ingawa waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo ni pamoja na raia kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Ufaransa, Canada, Australia, Marekani, Uingereza, Ghana na kwingineko.
Pamoja na majeshi na polisi wa Kenya kuzingira jengo hilo tangu saa chache baada ya tukio, taarifa zinadai baadhi ya magaidi waliokuwa katika jengo hilo, walitoroka kupitia mtaro wa maji machafu uliokuwa chini ya jengo hilo na huenda watu wengi zaidi wakawa wamepoteza maisha ikiwemo mateka waliodaiwa kushikiliwa na magaidi hao ndani ya jengo hilo.
Shambulio hilo ni la pili kwa ukubwa nchini humo likihusisha kikundi cha al Shabaab chenye ushirika na al Qaeda ambao wanadaiwa kuhusika na shambulizi kubwa lililotokea mwaka 1998 katika Ubalozi wa Marekani nchini humo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 220.

CHANZO: HABARI LEO