NCHI za Tanzania na Burundi, kwa mara
nyingine zimetengwa na wenzao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
baada ya marais wa Kenya, Uganda na Rwanda kukutana mjini Kigali jana.
Marais hao walitarajia kujadili namna ya kuimarisha Jumuiya ya Afrika
Mashariki kupitia uimarishwaji wa miundombinu, uchumi, biashara pamoja
na kuweka mikakati ya shirikisho la kisiasa.
Kitendo cha kuziacha Tanzania na
Burundi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kinazidi
kutia shaka mtangamano wa jumuiya hiyo.
Nchi hizo mbili zimeshaeleza
kusikitishwa na muungano wa nchi hizo tatu, ambao zimesema unakwenda
kinyume cha makubaliano na mkataba wa EAC.
Katika mkutano huo, marais hao, Paul
Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya,
pamoja na mambo mengine, walitarajia kusaini makubaliano ya kuanzisha
kituo kimoja cha kukusanya ushuru kinachotarajia kurahisisha uchukuzi wa
bidhaa kutoka Mombasa nchini Kenya, Uganda hadi Rwanda.
Aidha Sudan Kusini ilialikwa ikiidhinishwa kama mshirika katika kikao hicho.
Mkutano huo unakuja baada ya ule
uliofanyika mjini Kampala, Uganda, Juni mwaka huu na mwingine
uliofanyika Mombasa, Agosti, ambako viongozi hao watatu walipendekeza
kupanuliwa kwa Bandari ya Mombasa, ili kuwezesha uharaka wa bidhaa
kupitishwa katika kuhudumia kanda nzima.
Mkutano mwingine wa marais wa nchi 15
za Afrika, ikiwamo Tanzania, utafanyika leo nchini hapa, katika
kongamano la siku nne ambalo linatarajiwa kuweka kipaumbele kwa
uimarishwaji wa huduma za internet katika mataifa hayo.
Kwa mujibu ya waandaaji, zaidi ya
wajumbe 1,500 watahudhuria mkutano huo, chini ya uenyeji wa Rais Paul
Kagame na Dk. Hamadoun I. Toure, Katibu Mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa
Mawasiliano ya Kiteknolojia (ITU).
-Mtanzania