Friday, September 27, 2013

UPDATES":Barabara Tanzania zapitisha biashara haramu


BARABARA za Tanzania zimekuwa zikitumika kupitisha biashara haramu ya binadamu. Kauli hiyo imetolewa na Rais Jakaya Kikwete, ambapo alifafanua kwamba hakuna shughuli za biashara haramu ya binadamu inayofanywa Tanzania.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema Serikali yake itaendelea kushirikiana na nchi jirani kuhusu chimbuko la biashara hiyo, na katika kuchukua hatua za kukomesha vitendo hivyo haramu.
Alitoa msimamo huo wa Tanzania juzi, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Daniel Yohannes.
Ujumbe huo ulikutana na Rais Kikwete mjini New York, ambako amefikia kwa ziara yake ya kikazi nchini Marekani.
Yohannes na wenzake walikuwa wanamwelezea Rais Kikwete maendeleo ya ombi la Tanzania la awamu ya pili ya misaada ya maendeleo, baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza.
Katika mazungumzo hayo, Yohannes alitaka kujua hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Rais Kikwete, kukabiliana na baadhi ya mambo yanayojitokeza kuwa changamoto katika utekelezaji wa miradi ya MCC, kupitia Akaunti ya Milenia Tanzania (MCAT).
Baadhi ya changamoto ambazo Yohannes amezitaja ni pamoja na nini kinafanyika kuhusu Shirika la Umeme (TANESCO), juhudi za kupambana na rushwa na jinsi gani ya kukabiliana na biashara haramu ya binadamu.
Rais Kikwete ametoa majibu ya changamoto zote tatu na kumweleza Yohannes kuwa biashara haramu ya binadamu haifanyiki wala kuanzia katika Tanzania na kuwa inaanzia Ethiopia inapitia Kenya, Tanzania, Malawi na kwenda hadi Afrika Kusini.
“Wanakusanya watu katika Ethiopia na kuna mtu anapewa fedha na watu hao wanaokusanywa. Wanakuja Kenya na kuna mtu wa kuwapokea na kuwahudumia, wanakuja Arusha na hatimaye wanaingia Malawi na Afrika Kusini.Katika Tanzania wanapita tu na kuna wakati tulipata kukamata Waethiopia kiasi cha 19,000 na tukawarudisha kwao kwa gharama yetu,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kutoka Ethiopia watu hawa wamekuwa kama mto usiokauka maji. Hivyo, sisi katika Tanzania tunafanywa kama njia ya kupitia tu. Ni kweli wako mawakala lakini kwa hakika biashara hii haifanyiki katika Tanzania. Inafanyika kwingine na nchi yetu inafanywa kama njia tu. Kuna wakati nilipata kuzungumza na viongozi wa Ethiopia na Kenya kuhusu suala hilo lakini bado tutaendelea kulifuatilia.”
Rais Kikwete aliendesha kikao chake cha kwanza kama Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Nchi za Umoja wa Afrika Kuhusu Mazingira (CAHOSCO).
Rais aliendesha kikao hicho Jumanne wiki hii, katika Ofisi za Ubalozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU), katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.
Ubalozi wa Kudumu wa AU una hadhi ya watazamaji UN. Alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Nchi Wanachama wa AU kuhusu Mazingira mwanzoni mwa mwaka huu, baada ya kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Meles Zenawi, aliyefariki Septemba mwaka jana.
source:habari leo