Tuesday, September 10, 2013

SPIKA WA BUNGE NDUGAI AJIGAMBA KUMTOA FREEMAN MBOWE BUNGENI

*Asema wanaompinga ni mbumbumbu wa kanuni za Bunge
NAIBU Spika, Job Ndugai ametetea uamuzi wake wa kuagiza kutolewa ndani ya ukumbi wa Bunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akisema alikuwa sahihi.


Mabishano hayo ambayo yalisababisha kuibuka kwa vurugu bungeni yalitokea mwishoni mwa wiki, muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu, ambapo kiongozi huyo wa Bunge aliruhusu mjadala kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uendelee.


Kutokana na hali hiyo, Mbowe alisimama kutaka kutoa ufafanuzi juu ya mjadala huo, lakini Ndugai alimzima na kumtaka kukaa chini, jambo ambalo halikumfurahisha Mbowe na kumfanya agomee agizo lake.


Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Ndugai alitumia muda mwingi kutetea uamuzi wake na kukosoa hoja za watu wanaompinga juu ya uamuzi wake huo.


Ndugai alisema katika kikao hicho, Mbowe alifanya jeuri kubishana na kiti na kueleza kuwa kanuni za Bunge zinasema hakuna mbunge yeyote atakayesimama kuzungumza bila kuruhusiwa na kwamba uamuzi wa kiti ndiyo wa mwisho.


Ndugai alisema wanaomtuhumu kwamba hakutenda haki kumuamuru Mbowe akae chini, wanafanya hivyo kwa vile hawajui kanuni za Bunge.


Ndugai alisema kwa mujibu wa kanuni, ni Rais wa Jamhuri pekee ndiye anayeruhusiwa kulihutubia Bunge kwa wakati anaoona yeye unafaa, lakini si mbunge.


“Hata rais mwenyewe ni lazima amwandikie barua spika, huu ndiyo utaratibu lakini si mbunge au waziri anayeruhusiwa kusimama kwa wakati anaoutaka yeye kuzungumza akaruhusiwa, ni lazima ataomba ruhusa kwa Spika na kama ipo nafasi ya kufanya hivyo Spika atamruhusu, kama haipo hataruhusiwa.


Alipoulizwa kwamba haoni kama alivunja kanuni kwa kumzuia Kiongozi wa Upinzani bungeni wakati kanuni za mabunge ya Jumuiya ya Madola zinatoa upendeleo kwa kiongozi huyo na waziri mkuu ndani ya Bunge, Ndugai alisema:


“Katika vikao vya Bunge, uamuzi wowote wa Spika unakuwa wa mwisho na hauwezi kupingwa na mbunge au waziri yeyote.


“Mbowe nilimuomba kwa heshima sana atupishe kwanza, nilimuelekeza karibu mara tatu…lakini mtu mzima anavunja utaratibu.


“Huyu Mbowe amejivunjia heshima mwenyewe, hata kanisani anayeendesha ibada ni mtu mmoja tu, na wengine wanapaswa kufuata utaratibu.


“Kwanza Mbowe alijitoa mwenyewe kwenye orodha kwa maandishi na ninayo hapa.... yeye na Halima Mdee, sasa alisimama kufanya nini kama sio ujeuri?


“Kanuni anazijua mimi ningemruhusu tu, lakini kwa ujeuri hakufanya hivyo. Kuna taratibu za bunge, mbunge anakaa chini pale Spika anaposimama na wasome kanuni, sasa hapo mjeuri ni nani? 


“Tujifunze kanuni haiwezekani mtu yeyote asimame saa yoyote, kila mmoja hawezi kufanya anavyotaka, kuna taratibu zake, kiti kikimuona atapewa nafasi kama ipo na iwapo kiti kikiridhika,” alisema Naibu Spika