![]() | Leseni ya udereva. |
Baadhi ya
wahamiaji haramu, wamekuwa wakitumia mbinu ya kupiga picha na viongozi
wa juu wa Serikali na kuzitumia kama ‘kibali’ cha kukaa nchini.
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, alisema hayo jana
alipozungumza na waandishi wa habari na kuonya kuwa mbinu hizo
zimebainika na hazikubaliki.
“Kuna
watu wasio raia ambao wamekuwa wakipiga picha na viongozi… hiyo
haitakuwa dawa, hata mimi niliingia katika mtego na raia wa India ambaye
katika kusalimiana, alipiga picha kumbe ni mhamiaji haramu, mtu huyo
tulimwondoa mara moja,” alisema.
Alitaka wahamiaji haramu waliojificha, kurejea kwao au kuhalalisha ukaaji wao nchini kwa kufuata utaratibu wa kimataifa.
“Tunawapenda
sana majirani zetu na tunawapenda marafiki zetu, lakini watu wanaotaka
kuishi nchini ni lazima wazingatie utaratibu wa kimataifa. Vivyo hivyo
kwa Watanzania wanaokaa nchi zingine,” alisema.
Alisema
wakifuata utaratibu wa kimataifa, watasaidia kuongeza usalama wa nchi
kujua ina raia wa nchi gani na hata nchi zao, kujua raia wake walio nje
ya nchi.
Alionya
Watanzania wanaopokea na kuhifadhi watu wasiowafahamu, kuwa mbali na
matatizo ya kisheria yanayoweza kuwakuta, lakini pia wanahatarisha amani
ya nchi.
“Kila mtu
anatakiwa kuwa macho na wageni ambao hawawafahamu hasa katika kipindi
hiki ambacho usalama wa dunia uko shakani,” alisema.
Nchimbi
alitolea mfano wa gaidi wa Kingereza, ambaye aliishi nchini kwa
kubadili majina na alipenya hadi kupewa kadi ya mpiga kura.
“Pamoja
na kupongeza watendaji kwa kumkamata gaidi huyo, lakini ukweli tutakuwa
tunashangaza… mpaka huyo mtu kapewa leseni ya Tanzania na kadi ya
kupigia kura?” Alishangaa.
Nchimbi
pia alitaka viongozi wa serikali za mitaa nchini watimize wajibu wao wa
kuhakikisha wanakuwa macho na wahamiaji haramu katika maeneo yao.
“Sasa
tutaanza kuulizana na kuchukuliana hatua na wenyeviti na watendaji wa
mitaa, kwani haiwezekani eneo moja tukamate wahamiaji haramu 30 au 40 na
kuwachukua wao tu, wanatakiwa kuwajibika kwa hili,” alisema.
Wakati
huo huo, ugomvi wa wapenzi, umesababisha raia wa Tanzania, Martina
Pius, kutoboa siri kuwa baba mtoto wake, Fidele Ndayiragijimana (25) ni
mhamiaji haramu kutoka Burundi.
Akisimulia
kisa hicho jana, Kaimu Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dodoma, Naibu Kamishna
Proches Kuoko, alisema kwa sasa Ndayiragijimana ambaye alikuwa akiishi
kijiji cha Itiso wilayani Chamwino, anashikiliwa katika Ofisi ya
Uhamiaji Mkoa wa Dodoma.
Kwa
mujibu wa Kuoko, Ndayiragijimana alikuwa akiishi katika kijiji hicho
tangu mwaka 2009 na katika mapenzi yao na Martina, walibahatika kupata
mtoto.
Alisema Ndayiragijimana alikuwa akifanya kazi kwa mkulima na amekuwa akijitambulisha kwa bosi wake kuwa mzaliwa wa Kigoma.
Kuoko
alisema baada ya kusikia Operesheni Kimbunga imeanza, Ndayiragijimana
alirudi Burundi akachukue pasipoti na kuingia nchini na kuishi kihalali.
Hata
hivyo, Ndayiragijimana alipata hati ya muda ya Burundi, ambayo Kuoko
alisema aliitumia kuingia nchini kupitia mpaka wa Manyovu, Kigoma na
kupata kibali cha mwezi mmoja cha kuingilia nchini.
Hata
hivyo, kibali hicho kilimaliza muda wake Septemba 6 na alipaswa kurejea
kwao, jambo ambalo hakulifanya na kuendelea kuishi kwa siri, mpaka
Martina alipofichua siri hiyo.
Mhamiaji
mwingine aliyekamatwa ni Husna Zekwana (26), raia wa Uganda, aliyekutwa
na mtoto wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja aliyeingia nchini akitoka
Kampala kwa kupitia mpaka wa Horohoro, Tanga.
Ofisa
Uhamiaji huyo alisema Husna alikutwa na hati ya kusafiria isiyo yake,
bali alipewa na kondakta wa basi la Smart ili avuke na kisha amrudishie
baada ya kufika Dodoma.
Akizungumzia
Operesheni Kimbunga Awamu ya Pili, Dk Nchimbi alisema wanapanga upya
ratiba, lakini nguvu ya kamatakamata inaweza kupungua kwa asilimia 70.
Katika
awamu ya kwanza, kwa mujibu wa Dk Nchimbi, wahamiaji haramu 12,604
walikamatwa na kati yao, Wanyarwanda ni 3,448, Warundi 6,125, Waganda
2,496, Wakongo 589, Wasomali 44, Myemeni mmoja na raia wa India mmoja.
Alisema
watuhumiwa 212 wa unyang’anyi wa kutumia silaha walikamatwa, pia mabomu
10 ya mkono, silaha tofauti 61, risasi 665 na mitambo miwili ya
kutengeneza magobori.
“Tulifanya
msako hata katika hifadhi za Taifa ambako ng’ombe 8,226 walikamatwa na
zaidi ya Sh milioni 32.5 kupatikana kama tozo kutokana na faini ya
ng’ombe walioachwa katika hifadhi ya Taifa,” alisema.
Nchimbi
alisema pia walikamata nyara za Serikali ikiwamo ngozi ya duma, mbili za
swala na vipande 10 vya nyama vinavyodhaniwa kuwa nyara za Serikali.
Pia walikamata mbao 2,105, magogo 86, bangi kilo 77 na vipande viwili
vya meno ya tembo.
Kuhusu
wakimbizi wa Burundi zaidi ya 200,000 ambao wako nchini tangu mwaka
1972, Nchimbi alisema kazi ya kutoa uraia kwa watu hao ilisitishwa.
Sababu ya
kusitishwa, ni hatua ya baadhi ya wabunge na wakuu wa mikoa kukataa
kuwapokea baada ya kutokea vitendo vya uhalifu maeneo ya Kaskazini.
“Pamoja
na kuwa tulikubaliana na Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR),
tulisitisha kazi hiyo na sasa Serikali inatafakari njia mwafaka kwa kuwa
kama mpango huo ungeendelea, basi ingekuwa Serikali yenye kiburi,”
alisema.