Thursday, September 5, 2013

KCMC yamnasa daktari feki akiandaa upasuaji














Moshi. Taharuki na hofu imewakumba wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya uongozi wa hospitali hiyo kumkamata daktari feki aliyekuwa na nia ya kumfanyia upasuaji wa ngozi, mmoja wa wagonjwa aliyekuwa hospitalini hapo na kutapeliwa Sh200,000
Alikamatwa katika wodi ya upasuaji akijinadi kwamba ni daktari wa watoto ametambuliwa kuwa ni Alex Sumni Massawe, ambaye alikamatwa jana asubuhi na makachero wa Polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia baada ya uongozi wa hospitali hiyo kumuwekea mtego.
Kabla ya kukamatwa kwa Massawe, Mama mzazi wa kijana aliyetakiwa kufanyiwa upasuaji wa ngozi, Pamvelina Shirima alikutana na daktari huyo katika baa moja maarufu mjini hapa (jina limehifadhiwa) na kumtaka ampatie Sh200,000 ambazo atazitumia kuharakisha mwanae Makasi Tipesa afanyiwe vipimo .
Ofisa Uhusiano wa Hospitali hiyo,Gabriel Chisseo aliwaambia waandishi wa habari kwamba Massawe aliwekewa mtego na uongozi wa Hospitali ya KCMC kutokana na baadhi ya wagonjwa kuripoti kutapeliwa na daktari huyo feki. Alisema mama wa mgonjwa alipewa taarifa na rafiki yake kuwa anaweza kumpatia daktari atakayemsaidia kupata huduma kwa haraka,ambapo alimkutanisha na Massawe kwenye baa hiyo na kumfanyia mtoto huyo vipimo baa.
“Alex Massawe tulimkamata jana asubuhi akiwa wodi ya upasuaji baada ya kupokea kiasi cha Sh200,000 kutoka kwa Pamvelina Shirima ambaye alimleta mwanae afanyiwe upasuaji wa ngozi. Tunawataka wagonjwa wote kufuata taratibu ikiwamo kutokubali kurubuniwa na watu ambao hawajavaa sare wala vitambulisho rasmi ,” alisema Chisseo.
Kufuatia tukio hilo,Hospitali ya KCMC imethibitisha kuwa mtu huyo alikamatwa ndani ya hospitali hiyo, si mwajiriwa wao na wala hakukutwa na sare wala kitambulisho cha kitengo chake cha kazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema polisi itamfikisha mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika.