Friday, September 6, 2013

JWTZ: Kikosi chetu DRC ni cha kulinda amani, si kupigana na Rwanda





Msemaji wa Jeshi laDar es Salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, (JWTZ) limeeleza kuwa Tanzania haikupeleka kikosi cha jeshi hilo kwenye Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)(Monusco) kwa ajili ya kupigana na Rwanda, bali kusaidia kulinda amani.
Ufafanuzi huo umekuja siku mbili baada ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na Rais Paul Kagame wa Rwanda, kufuatia baadhi vyombo vya habari vikiandika habari jinsi JWTZ kilivyopambana na waasi wa Kikosi cha M23 na kukisambaratisha, sambamba na malumbano kati ya Tanzania na Rwanda.
Askari wa Tanzania na wale wa Afrika Kusini wako DRC kwa kazi ya kulinda amani. Malawi bado haijapeleka majeshi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba alisema,“Kikosi cha Tanzania kilichopo DRC ni sehemu ya Kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kilichotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (Monusco) na kinafanya kazi chini ya komandi ya Monusco.”
Alifafanua kuwa kazi ya kikosi hicho ni kuzuia waasi kujitanua, kuvunja nguvu yao pamoja na kuwapokonya silaha, huku akisisitiza kuwa sio kweli kuwa Tanzania ilikuwa ikipigana na Rwanda au waasi wa M23, kama ambavyo imekuwa ikielezwa.
“Ridhaa ya kikosi chetu kwenda DRC ilikubaliwa pia na Rwanda, nchi ambayo ni mwanachama wa nchi za maziwa makuu. Aidha Rwanda imesaidia kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha watu,vifaa na zana nchini kupitia nchi hiyo kwenda DRC,” alisema.
Alisema kuwa vikosi hivyo ambavyo mbali na Waasi wa M23 pia vimekuwa vikipambana na vikosi vya Waasi vya ADF na FDLR, kwamba bado vinaendelea kulinda amani nchini DRC na kama kunaibuka mapambano navyo hulazimika kujibu mapigo.
Kikosi cha Munusco kilianza kupambana na waasi, Agosti 27, mwaka huu na askari wa JWTZ, Khatibu Mshindo alikuwa miongoni mwa waliouawa kwa kupigwa bomu na M23 Mjini Goma ulioko Mashariki mwa DRC. baada ya kuzuka mapigano makali.