RAIS Jakaya Kikwete ameiagiza Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Kitengo cha Magonjwa ya Akili na Tume ya
Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, kuwasaidia waathirika wa
dawa hizo.
Rais alitaka Wizara na tume hiyo,
kushirikiana na Kituo cha Ushauri cha Pili Misana Foundation, ambacho
kinawasaidia waathirika wa dawa hizo, ili kiwahudumie watu wengi zaidi
nchini.
Alisema hayo juzi Ikulu Dar es Salaam,
alipokutana na vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya, ambao
wamepata ushauri nasaha na usaidizi kutoka katika kituo cha Pili Misana
kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.
“Jamii lazima ishiriki katika utatuzi wa
jambo hili, ni tatizo kubwa na linamgusa kila mtu na inabidi wote
tushiriki katika kulipiga vita,” alisema Rais na kumpongeza Misana na
Zacharia Hans Pope, ambaye ndiye mfadhili wa kituo hicho.
Kituo hicho tayari vijana wapatao 203,
ambao wamepatiwa huduma ya ushauri na kuachana na dawa za kulevya na
kurudia katika shughuli zao za kimaendeleo.
Rais Kikwete amesema tatizo la dawa za
kulevya ni la muda mrefu, lakini hapo awali lilikuwa halisikiki sana kwa
sababu jitihada za kuzuia dawa hizo zilikuwa hazitangazwi wala
kufuatiliwa.
“Sasa hivi juhudi mbalimbali za
kupambana na dawa za kulevya zinatangazwa na kusikika na pia taarifa
nyingi zinazohusu dawa za kulevya zinawekwa wazi kwa jamii,” alisema
Rais na kueleza kuwa taarifa nyingi zinawekwa wazi na kutangazwa, ili
kushirikisha jamii kupambana na tatizo hilo.
Vijana 35 kutoka katika nyanja
mbalimbali za kitaaluma, elimu na kijamii na umri tofauti kutoka miaka
14 hadi miaka 53, walifika Ikulu juzi kuzungumza na Rais.
Kituo hicho kinahudumia watu wenye
jinsia tofauti, wake kwa waume kutoka sehemu mbalimbali nchini. Rais
Kikwete alisema Serikali inafanya jitihada kubwa za kusaidia vijana
mbalimbali na bado itaendelea kutoa msaada huo, huku juhudi mbalimbali
za kupambana na dawa hizo zinaendelea.