Wakati bilionea mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite yanayopatikana Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, marehemu Erasto Simon Msuya (43) akitarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwao mtaa wa Kairo, Mji mdogo wa Mirerani, polisi imewatia mbaroni watu wawili wakihusishwa katika mtandao uliofanya mauaji ya mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara huyo anayemiliki vitega uchumi
kadhaa katika miji hiyo, aliuawa Agosti 8, mwaka huu katika eneo la
Mjohoroni wilayani Hai baada ya kumiminiwa risasi zaidi ya 20 za bunduki
ya kivita aina ya SMG.
Habari zilizopatikana jana Arusha, zilidokeza kuwa
washukiwa hao walikamatwa siku ya tukio huko Sanyajuu wilayani Siha,
kilomita chache kutoka mahali ilipotelekezwa pikipiki iliyotumika katika
mauaji hayo.
Pikipiki hiyo mpya ilitelekezwa katika Kijiji cha
Olkolili baada ya kupata pancha gurudumu la mbele na watu waliokuwa
wakiitumia waliiacha na kuamua kutembea kwa miguu.
Habari zinadai kuwa watu hao wawili sio
waliomfyatulia risasi mfanyabiashara huyo bali wana ‘taarifa muhimu’
zinazohusiana na mpango mzima wa mauaji hayo na mtandao wa watuhumiwa
waliohusika.
Inadaiwa kuwa baada ya wauaji wa mfanyabiashara
huyo kutelekeza pikipiki hiyo, ‘waliwezeshwa’ kutoroka kupitia Wilaya ya
Simanjiro na baadaye kuingia jijini hapa ingawa hawajulikani mahali
waliko.
“Ni kweli kuna watu wawili walikamatwa na
wanashikiliwa kule Makao Makuu ya Polisi Moshi na kila siku wanaletwa
hapa Arusha kwa ajili ya uchunguzi wa kuwatafuta wahusika hasa,”
alidokeza polisi mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kuelezea zaidi baada ya simu yake kutokupatikana.
Ofisa huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe,
alisema hata hiyo jana, timu ya wapelelezi kutoka Moshi wakiongozwa na
RCO Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi walikuwapo jijini hapa na watuhumiwa
hao.
Uchunguzi zaidi wa polisi kuhusu mmiliki halali wa
pikipiki iliyokuwa ikitumiwa na vijana wawili waliotekeleza mauaji
hayo, zimebaini kuwa bado inamilikiwa na kampuni moja ya Dar es Salaam
iliyouza pikipiki hiyo.
Habari zaidi zinadai kuwa pikipiki hiyo
ilinunuliwa mahususi kwa ajili hiyo na mwanamke mmoja ambaye hafahamiki
na ilinunuliwa katika duka ambalo ni tawi la kampuni iliyoingiza
pikipiki hiyo lililopo Arusha.
Mfanyabiashara huyo ambaye anatarajiwa kuzikwa
kesho, huko Mirerani, aliuawa baada ya kuitwa kwa simu na wauaji
waliojifanya ni vijana wenye madini ya Tanzanite waliotaka kumuuzia
marehemu.