Monday, August 5, 2013

SITTA "WABUNGE VITI MAALUMU HAWANA UMUHIMU WOWOTE"







Wiki moja baada ya kukaririwa akisema baadhi ya wabunge wa CCM ni mizigo na kwamba hawana mchango wowote bungeni na wala hawatembelei majimbo yao wakisubiri kubebwa na chama, Spika wa Bunge wa zamani, Samuel Sitta amewageukia wabunge wa Viti Maalumu akisema hawana umuhimu wowote. 
Akizungumza kwa simu juzi, Sitta ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema: “Ninakerwa sana na mfumo wa Viti Maalumu, kwanza sioni umuhimu wa mfumo huu kuendelea kuwepo katika Katiba Mpya. Hawana umuhimu wowote.”
Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Nyamikoma, Kata ya Busega Mkoa wa Simiyu Julai 29, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuimarisha uhai wa chama, Sitta aliwajia juu bila ya kuwataja baadhi ya wabunge wa CCM.
“Wanakwenda bungeni hawachangii, hawana hata hoja za kuchachafya upinzani, hawachangii, hawa ni mzigo,” alisema Sitta na kuongeza: “Wapo baadhi ya wabunge, hawajawahi hata siku moja kwenda kwenye majimbo yao kuwatembelea wananchi waliowachagua... Inawezekana hata wapiga kura wakawa wamewasahau. Hawa hawafai hata kuchaguliwa wakiomba tena kura.”
“Rais Jakaya Kikwete amejitahidi sana kuleta mabadiliko, ameleta mafanikio ya uchumi na mambo mengi. Inatakiwa wabunge waende wakawaeleze wananchi maendeleo haya, inawezekana hawayajui lakini watu hawaendi jimboni, wananchi watayafahamu vipi haya maendeleo?”
Juzi, akizungumzia wabunge wa Viti Maalumu, Sitta alisema... “Wengi wao hawachangii chochote na mbaya zaidi hakuna wa kuwahoji chochote kama wabunge wanavyorudi jimboni.
“Ikifika wakati wa posho wapo. Sisemi kama naumia wao kuchukua posho.... hawa wanachukua posho wanawajibika kwa nani? Nani anahoji utendaji wao na zaidi itakapokuja Katiba Mpya ya kuwawajibisha wabunge wazembe, hawa watawajibishwa wapi?”
“Rasimu ya Katiba Mpya isiwaruhusu hawa... hawa nao ni mzigo mwingine. Wakifika bungeni hawachangii chochote, hawawezi kuwajibishwa na yeyote kwa mfumo uliopo na pia hawawajibiki popote, sasa huu si mzigo?”
Walikwishaanza mkakati
Hata hivyo, Juni 9, mwaka huu, ikiwa ni wiki moja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kutangaza Rasimu ya Katiba huku ikifuta Viti Maalumu, wabunge wanawake walianza kuweka mikakati ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa lengo la kukamata majimbo.
Kwa  mara ya kwanza, wabunge hao wa Viti Maalumu walikutana kwa siku mbili kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa, Dodoma lengo likiwa ni kujadili mikakati mbalimbali ya kupambana  jimboni.
Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake, Anna Abdallah alisema wanaweka mikakati kuwawezesha kusimama wenyewe kwenye majimbo mwaka 2015 hasa baada ya kufutwa kwa Viti Maalumu katika rasimu.

Mbunge huyo alikiri kuwa Viti Maalum haviwapi sifa stahiki kama wabunge kwa kuwa hawana uwakilishi wa moja kwa moja kwa wananchi. Alisema bila kuangalia nafasi za vyama, suala la Viti Maalumu linawabagua na wabunge wa majimbo.
Msimamo wa wabunge wa Viti Maalumu
Baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutangaza rasimu, baadhi ya wabunge wa Viti Maalumu walizungumzia hatima ya nafasi hiyo huku wengi wakionekana kuunga mkono kufutwa kwake.
Mmoja wao ni Grace Kihwelu (Chadema), ambaye alisema: “Ninachotaka wabunge twende hukohuko jimboni tukapambane kwani inaleta heshima. Hii ya kuteuliwa inatunyima raha.”
Mbunge mwingine wa Chadema kutoka Zanzibar, Mariam Msabaha alisema: “Mimi nilikuwa wa kwanza kupingana na haya ya Viti Maalumu ndiyo maana nikasimama moja kwa moja Jimbo la Jang’ombe kupigana. Sikutaka kuteuliwa.”
Catherine Magige (CCM), alisema: “Viti Maalumu havionyeshi ufanisi wa moja kwa moja na sehemu kubwa mbunge ndiye anayeonekana kwa wananchi.”
Mbunge mwingine wa Viti Maalumu (CCM), Martha Mlata alisema mfumo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba utarudisha heshima kwa wabunge wanawake kwa kuwa wanakwenda kupambana katika majimbo.
Ritha Kabati wa CCM alielezea kufurahishwa kwake na Tume ya Warioba kuondoa Viti Maalumu... “Vilikuwa vinatudhalilisha, watu walikuwa hawatupi thamani halisi kama wabunge.”
Suzan Lyimo wa Chadema alisema: “Nimeupenda uamuzi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wakati mwingine Viti Maalumu vilikuwa vinatolewa kwa rushwa na sisi wanawake ndiyo ilikuwa inasemwa vibaya. Sasa ni bora huko katika majimbo tukapambane.”

Source:Mwananchi