Wednesday, August 21, 2013

Picha hii imezua mjadala na CHADEMA kulazimika kuitolea ufafanuzi

Yadai Ofisa wa Polisi anayeonekana kwenye picha, alikuwa akiwaelekeza watu wasogee pembeni kwanza, akimwambia Slaa asubiri kidogo watengeneze njia 'vizuri' apite!
Tangu mapema sana asubuhi, tumepokea simu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, watu tofauti, wakionesha concerns zao juu ya taarifa kuwa ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi ameonekana kwenye picha 'akimdhibiti' Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willbroad Slaa.

Picha na maelezo yake (caption) yameonekana kuwasononesha na kuwatisha watu wengi.

Ili kusaidia jamii na kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea, iwapo usahihi wa tukio hilo hautaelezwa, tumeona ni vyema kwa nafasi yetu kuweka kumbukumbu sawa.

USAHIHI; Kama ilivyo ada ya misafara ya CHADEMA, hasa inapohusisha viongozi wakuu, viongozi (watendaji waandamizi) wengine wa kitaifa, wabunge na viongozi wengine wa chama katika maeneo husika, huwa ina hamasa, shamrashamra na mapokezi makubwa kila mahali kunapofanyika mikutano au shughuli ya kichama.

Katibu Mkuu, Dkt. Slaa na timu yake walipotua Mpwapwa kwa helkopta siku ya Agosti 18, mwaka huu, alilakiwa na umati mkubwa wa watu, wakitaka kumsalimia na kumkumbatia. Wakifurahia ujio wa mmoja wa viongozi wakuu wa chama katika eneo lao, kwa ajili ya kuendesha Mabaraza Huru ya Rasimu ya Katiba Mpya, katike eneo hilo.

Katika hali kama hiyo, walinzi, wakiwemo askari polisi, walikuwa 'concerned' na hali ya usalama, maana 'lolote' laweza kutokea. Ofisa wa Polisi anayeonekana kwenye picha, alikuwa akiwaelekeza watu wasogee pembeni kwanza, akimwambia Daktari asubiri kidogo watengeneze njia 'vizuri' apite, maana watu wote wale kumfuata na kumkumbatia ingeweza kuwa hatari.

Kama anavyoonekana, Dkt. Slaa naye alikuwa akijaribu kumwambia yule askari kuwa awasaidie wale watu bila kuharibu utaratibu wa yeye kusalimiana na wananchi wake, ambao hujaa kumlaki kwa nia njema, bila kukodiwa wala kusombwa.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa. Hakukuwa na 'kudhibitiana', bali kulikuwa na kuongozana.

Timu ya Katibu Mkuu, kama ilivyo kwa Mwenyekiti Freeman Mbowe, kwa kutumia usafiri wa chopa, inaendelea na ratiba ya kuendesha Mabaraza Huru ya Rasimu ya Katiba Mpya, ambapo muda huu timu ya Mwenyekiti imeshaingia Mkoa wa Katavi, kutokea Tabora na timu ya Dkt. Slaa iko Morogoro!

Maelfu ya Watanzania wanaendelea kupata fursa ya kushiriki moja kwa moja, kutoa maoni yao kwenye mabaraza hayo, yanayoendeshwa kwa njia ya wazi kwenye mikutano ya hadhara.

Nawe unaweza kuendelea kutoa maoni yako ya katiba, kwenye Mabaraza Huru ya Rasimu ya Katiba Mpya, kupitia ujumbe mfupi kwenye namba 0789 248224 au email; chademamaoni@gmail.com