Monday, August 19, 2013

KAMATI YA BUNGE YAITAKA TRA KUTOA MAELEZO YA VIGEZO VILIVYOTUMIKA KUMPANDISHA CHEO ASIYESTAHILI.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Biashara na Viwanda imeitaka Bodi ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kutoa maelezo ya vigezo vilivyotumika kumpandisha cheo ofisa wake anayetuhumiwa kwa kushindwa kusimamia wajibu wake.
Ofisa huyo Tiagi Masamaki, awali alikuwa Kaimu Kamishina wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, wakati huo akikabiliwa na tuhuma kadhaa ikiwamo makontena kupotea mikononi mwake.
Kamati hiyo ambayo juzi ilifanya ziara TRA na kupewa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo baada ya kusikiliza maelezo ya maofisa ya mamlaka hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa aliibua hoja hiyo.
Mgimwa ambaye ni mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM), alisema kamati hiyo haijaridhishwa na mwenendo wa kuchukulia hatua wafanyakazi wa ngazi za chini huku wakubwa wakikumbatiwa na bodi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watumishi wanane walisimamishwa kazi wakituhumiwa kuhusika na upotevu wa kodi za serikali pamoja na tuhuma za rushwa kwa kushirikiana na mawakala wasio waaminifu kutoa makontena bandarini.
"Bodi itueleze wametumia utaratibu gani kumpa ukamishina Masamaki wakati anakabiliwa na tuhuma, hatukubali kumpromote (kumpandisha) mtu wakati ana madudu makubwa yamefanyika wakati akiwa anakaimu idara hiyo," alisema Mgimwa.
Mgimwa aliagiza Mwenyekiti wa Bodi kukutana nae Dodoma ili kamati ipewe ufafanuzi kuhusu suala hilo pamoja na mambo mengine. "Hivi ni kweli mtu anafanya madudu anapongezwa na bodi kwa kupewa ulaji, hatuwezi kufika na ndiyo maana tulisema tunataka kikao hiki awepo mwenyekiti wa bodi bila kukosa."
Alisema kuna matatizo kwa baadhi ya maofisa wa TRA kudaiwa kushiriki kupitisha bidhaa katika bandari bubu.
Mgimwa alisema baada ya kupewa taarifa ya kushushwa kwa shehena ya mafuta bandari bubu alifanya jitihada zake na kufanikiwa kupata picha dhidi ya tukio hilo ambalo lipo wazi katika ushushaji.
Alisema kwa sasa bandari imejiosha lakini tatizo kubwa lipo kwa TRA baada ya kubaini kuwepo kwa rushwa huku wengine wakilipia kodi milangoni.
Aliongeza kuwa kuna kampuni ambazo hazijalipa kodi kwa zaidi ya miaka 10 wakati kuna nchi duniani zinajiendesha kupitia bandari lakini kwa Tanzania bado ni tatizo.
Alisema wafanyabiashara wengi wamekwepa kulipa kodi huku akitoa mfano wa wauza chips katikati ya jiji.
Kamishina Idara ya Walipa kodi Wakubwa, Neema Mrema, alisema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya madeni hasa katika mashirika ya umma ikiwemo Tazara na ATCL kwa kutolipa kodi.
Hata hivyo, Mgimwa ameiagiza TRA kuhakikisha inatoa taarifa ya madeni yanayodaiwa katika mashirika ya umma na kampuni zilizokwepa kodi ili kamati ilifanyie kazi.
Naibu Kamishina wa TRA, Rished Bade, aliahidi kutoa taarifa kwa kamati hiyo baada ya maagizo ya kamati.  
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI