Tuesday, August 6, 2013

DR.MWAKYEMBE AICHARUKIA TAZARA...


Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameipa miezi mitatu menejimenti ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), kuwalipa wafanyakazi malimbikizo ya mishahara zaidi ya Sh. milioni 624.4 kwa wakati na wakishindwa waache kazi. 
Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa Tazara Mbeya ambao walimlalamikia kuwa tangu Mei hadi sasa hawajalipwa mishahara hali inayowafanya wakabiliwe na hali ngumu ya maisha.
 
Alisema miezi mitatu ikipita kama menejimenti itakuwa haijabadilika, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika na Mkurugenzi wa Mkoa wa Mbeya waandike barua ya kuacha kazi mara moja kabla hajawafukuza yeye.
 
Dk. Mwakyembe alisema serikali imeunda timu ya wataalam ambao ni wanasheria kutoka Tanzania na Zambia ambao watapitia upya mkataba wa Tazara kutokana na shirika kukabiliwa na matatizo mengi ambayo yanatokana na kuendeshwa kwa ushirikiano wa nchi mbili.
 
“Nimechoshwa na menejimenti ya Tazara, wanashindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi halafu wanaendelea kuwapo, mna mabilioni ya fedha mnawadai watu halafu mnashindwa kukusanya,” alisema Dk. Mwakyembe.
 
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania kanda ya Mbeya (Trawu), Christopher Kaziyo, alimweleza waziri kuwa wafanyakazi wanashangaa kutolipwa mishahara kwa miezi mitatu wakati kila mwezi kumekuwa na ongezeko la mizigo inayosafirishwa na Tazara.
 
Kaziyo alisema katika kipindi cha kuanzia Mei hadi Julai mwaka huu mizigo iliyosafirishwa ni tani 80,922 na kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni tisa zimelipwa na watu waliosafirishiwa mizigo hiyo. Alisema wafanyakazi pia wanalalamika michango yao ya NSSF kutopelekwa benki kwa zaidi ya miaka 10 jambo ambalo linazua maswali mengi wafanyakazi hao watakapostaafu.