Mazishi ya kifahari yanaandaliwa na familia ya marehemu Erasto Msuya, huku ikielezwa kuwa jeneza litakalotumika kubeba mwili wake linafunguka kwa kutumia ‘rimoti’.
Msuya aliyeuawa wiki
iliyopita, anazikwa leo huku familia ikitangaza kutokulipiza kisasi kwa
waliohusika, badala yake wamemwachia Mungu.
Kinachovutia
katika msiba huo ni jeneza lililobeba mwili wa mfanyabiashara huyo
lililoagizwa Nairobi, la aina yake huku likifunguliwa kwa kutumia
‘rimoti’.
Jeneza hilo lililoagizwa kutoka Kampuni
ya Montezuma & Monalisa Funeral Home, linafunguliwa kwa kubonyeza
kifaa maalumu hata mhusika anapokuwa mbali.
Hali
hiyo ilionekana kuwaacha na mshangao maelfu ya waombolezaji waliofika
kuaga mwili wakati wa ibada iliyofanyika nyumbani kwake, Kwa Iddi,
wilayani Arumeru.
Mfanyabiashara huyo aliyeuawa kwa
kumiminiwa risasi zaidi ya 20 na watu wasiojulikana, anazikwa leo
nyumbani kwao eneo la Kairo Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani
Manyara.
Kaka wa marehemu, Israel Msuya, alisema
jana kuwa mazishi hayo yatafanyika makaburi ya familia ya mzee Elisaria
Msuya ‘Kikaango’, baba wa marehemu Erasto.
Kwa
mujibu wa Kamati ya Maandalizi ya mazishi hayo inayoongozwa na kaka
mkubwa wa familia ya Msuya, Gady, zaidi ya Sh100 milioni zimepangwa
kugharimia shughuli za maombolezo na mazishi.
Jeneza
na gari maalumu la kubebea mwili wa marehemu yameagizwa kutoka Kampuni
ya Montezuma & Monalisa Funeral Home ya Nairobi, Kenya kwa gharama
ya Sh8 milioni.
Chakula, vinywaji, mapambo na
magari ya kukodishwa kutoka Arusha kwenda Mirerani na kurudi
yanatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh80 milioni.
Katika
hatua nyingine, polisi mkoani Arusha imeendelea kuwahoji
wafanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani,
wilayani Simanjiro, wakidaiwa kuhusika na kifo hicho.
Habari
zilizopatikana jana zinadai mfanyabiashara mmoja kijana ambaye aliibuka
ghafla kuwa tajiri mkubwa kutokana na biashara ya madini ya Tanzanite,
anashikiliwa Arusha kwa mahojiano.
Jana, kwenye viunga
vya Mji wa Mirerani watu walitangaziwa kuwa mfanyabiashara huyo, alikuwa
anashikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na kifo hicho.
Hata
hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas,
hakupatikana mara moja kuelezea suala hilo kwani simu yake ilipopigwa
ilikuwa haipatikani.
Marehemu ameacha mke na watoto
wanne, huku akiacha rasilimali nyingi ikiwamo jumba la kifahari
lililopo Sakina kwa Idd, hoteli maarufu za SG Resort na Mezza Luna
zilizopo Arusha.
Mwanananchi