Thursday, August 15, 2013

AGIZO LA SERIKALI:NI MARUFUKU KUTUMIA MIFUKO YA PLASTIKI...!!


Waziri  wa Nchi katika Ofisi  ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dk Terezya Huvisa  ametangaza leo kuwa Serikali imepiga marufuku ungizaji, utengenezaji, uuzaji, na utumiaji  wa mifuko ya plastiki.

Zuio hili linahusu mifuko yote ya plastiki ya kubebea bidhaa kutoka madukani, sokoni na majumbani.

Mifuko inayoruhusiwa ni ile yenye unene wa maikroni mia moja inayooza (bio-digradable) na  vifungashio vya bidhaa mbalimbali kama vile vifaa vya mahospitalini.

“Marufuku hii inapaswa kuzingatiwa na wenye viwanda, wenye maduka na wananchi kwa ujumla ili kutokomeza kuenea  kwa taka zinazotokana na mifuko ya plastiki kwenye mazingira,” amesema Waziri.

Ametoa agizo la kufanywa msako ili kuwakamata watakaokuwa wanaendelea kufanya biashara ya mifuko hii na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Amesema kuwa Serikali imechukua hatua hii ili kupunguza naa kuondoa kabisa tatizo la kusambaa na kutapakaa kwa taka za mifuko ya plastiki ambayo baada ya matumizi huishia kuyachafua mazingira.

Imeelezwa kuwa madhara yanayosababishwa na mifuko ya plastiki ni pamoja na uharibifu wa udongo unaotokana na kuunguzwa kwa plastiki hizi na hivyo kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu na wanyama, kutooza kiurahisi wa njia za kiasili (non-biodegradable) kuzagaa katika mito, maziwa, bahari na nchi kavu hivyo kuhatarisha maisha ya viumbe hai.