WAKATI Serikali ikiahidi kutazama upya tozo ya Sh 1,000 kwa laini za simu ili kupunguza mzigo kwa wananchi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema tozo hiyo si ya kuwaumiza wananchi bali mapato yake yatakwenda moja kwa moja kusaidia kueneza umeme vijijini.
Alisema hayo alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Songea juzi, katika ziara yake ya wiki moja mkoani Ruvuma, baada ya kuutembelea mkoa mpya wa Njombe.
“Ni kama vile tozo iliyoongezwa kwenye mafuta ya petroli, ambayo imetupa fedha nyingi kwenye Mfuko wa Barabara, za kuunganisha miji na mikoa na nyingi zimejengwa na zinaendelea kujengwa.
“Nani asiyetaka vijiji vipate umeme kama miji, ili usaidie kuondoa giza, uendeshe viwanda vidogo vidogo na usaidie kukuza uchumi? Wanaopinga tozo hii, hawatutakii mema,”alisema Pinda.
Bunge la bajeti lililomalizika mwezi uliopita, lilipitisha tozo ya Sh 1,000 kwa matumizi ya simu za mikononi, ili fedha zitakazopatikana zisaidie katika mpango mkubwa wa kueneza umeme vijijini unaoendeshwa na Wakala wa Umeme Vijijini, (REA). Kwa mkoa wa Ruvuma peke yake, vijiji vipatavyo 150 vitapatiwa umeme chini ya mpango huo.
Katika mikoa yote nchini kuna idadi inayotofautiana ya vijiji vingi vitakavyonufaika katika mpango huo. Umeme umo katika sekta ya nishati ambayo ni moja ya sekta sita zilizoteuliwa kutekelezwa chini ya mpango wa kuhakikisha matokeo makubwa yanapatikana sasa, wenye upeo wa miaka mitatu, kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2013/14. Sekta nyingine ni Kilimo, Uchukuzi, Maji, Elimu na Mapato.
Kabla ya mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alizindua Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Songea, kinachodahili zaidi ya wanafunzi 500 na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa mfundi stadi mbalimbali.
Awali Waziri Mkuu Pinda alisema bei ya mahindi kutoka kwa mkulima katika mkoa wa Ruvuma, itakuwa ni Sh 500 kwa kilo badala ya Sh 450, ili wakulima wahamasike kuuza mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Mkoa wa Ruvuma ni moja ya mikoa inayozalisha mahindi, chakula kikuu nchini kwa wingi na NFRA inatarajia kununua tani 50,000 kutoka katika mkoa huo.
NRFA imepangiwa kununua zaidi ya tani 200,000 nchini kote kwa ajili ya hifadhi ya chakula, kiwango kikubwa kuliko mwaka uliopita.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko la kimataifa katika kijiji cha Mkenda kwenye mpaka na Msumbiji, ikiwa ni moja ya masoko 48 yatakayojengwa mipakani kurahisisha biashara na kukabiliana na magendo. Leo Waziri Mkuu ataondoka Songea kurejea Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara yake mkoani humo.