Matendo, kawaida huwa yanaongea kwa sauti kubwa kuliko maneno. Japokuwa FC Barcelona imeshatoa kali kadhaa kwamba kiungo anayetakiwa na Manchester United, Cesc Fabregas, lakini ujumbe unaotolewa na klabu hiyo ya Catalunya unaweza usiwe na sauti kubwa, lakini wenyewe wameweka wazi Cesc hauzwi kwa bei yoyote.
United tayari wametuma ofa mbili kwa ajili ya kumsaini nahodha wa zamani wa Arsenal na manager David Moyes alikaririwa hivi karibuni mapema wiki hii kwamba mazungumzo yalikuwa yanaendelea, akitumaini kwamba boss mpya wa Barca Gerardo Martino angeweza kuwa anataka kumuuza kiungo huyo mwenye miaka 26 kwa fedha nyingi kadri iwezekanvyo. Lakini hilo sidhani litaweza kuwa.
Alipoulizwa Ijumaa iliyopita kuhusu uwezekano wa kumuuza Cesc wakati akitambulishwa, Martino alijibu: "Sitotaka kuingilia masuala ya kifedha ya klabu, lakini klabu tayari imeshakataa ofa mbili na nitaikataa ya tatu."
Kama hiyo haitoshi, makamu wa raisi wa klabu Josep Maria Bartomeu akaongeza kwamba;"Hatufikirii kabisa kumuuza Cesc, hatukwazwi na United kuendelea kumtaka mchezaji, tunajivunia kuona wachezaji wetu wanawavutia timu nyingine, lakini tuna furaha kuwa nae hapa. Ofa yoyote tutakayopokea, mchezaji huyu hauzwi."
Hivyo wakati mchezaji husika akiwa anaonekana kuchoshwa kwa kupigwa benchi mara nyingi na pia kuchezeshwa katika nafasi tofauti kwa klabu hiyo ambayo amekuwa akiisapoti, hataki kuondoka Barcelona. "Nataka kubaki Barca milele," kiungo huyo alikaririwa akisema mwezi wa pili mwaka huu, ingawa miezi miwili baadae alizomewa na mashabiki wake wa Barcelona wakati wa mchezo wa nusu fainali ya kombe la mabingwa wa ulaya, lakini bado alisema matamanio yake ni kubaki na kufanikiwa akiwa na Barca. "Cesc ana furaha na anataka kubaki hapa," mchezaji mwenzie na rafiki Gerard Pique alisema hivi karibuni, wakati boss wa zamani wa timu hiyo Tito Vilanova aliongeza mapema mwezi huu kabla ya kujiuzulu: "Ninafahamu kwamba tumepokea ofa, lakini mchezaji mwenyewe anataka kubaki."
Na Barca wanataka kuendelea kuwa na Cesc, huku Xavi akionyesha dalili za kuanza kuchoka na kucheza mechi mbili kwa wiki bila kuonyesha dalili za kuchoka. Pia Thiago Alcantara tayari ameondoka kwenda Bayern, Fabregas anaweza kupata muda mzuri wa kucheza kwenye kiungo kuanzia msimu ujao.
Lakini pia ujio wa Neymar unamaanisha Cesc atapata nafasi kidogo kucheza kwenye nafasi ya nyuma ya mshambuliaji, lakini kuondoka kwa Thiago ambaye alikuwa kama mbadala wa Xavi na Andres Iniesta katika kiungo - hivyo anaweza kuanza michezo mingi msimu ujao. Ikiwa watamuacha aondoke itabidi Barca waingie sokoni kutafuta mchezaji kama yeye au wampandishe kinda kutoka La Masia - na kuna wachezaji wachache wanaofanana nae.
Ingekuwa Thiago bado yupo Nou Camp, Barca wangeweza kumuuza Cesc na kuweka imani yao kwa Thiago, lakini baada ya kinda huyo kwenda kuungana na Guardiola, Fabregas sasa ni muhimu zaidi kwenye timu kuliko ilivyokuwa misimu uliyopita - Barca wamekuwa na utaratibu mzuri wa kupunguza deni lao, hivyo hawahitaji kuuza mchezaji ili kuweka hesabu za vitabu sawa. Lakini pia timu hiyo inasaka mabeki wa daraja la dunia hili kuimarisha nafasi ya ulinzi ambayo imeonekana kuwa dhaifu hivi karibuni, hivyo pia wanaweza wakamuuza Cesc ili kujiwezesha kutoa dau zuri ambalo litawawezesha kutoa ofa isiyokuwa rahisi kuikataa kwa aidha Chelsea wakiwa na nia ya kumsaini David Luiz, Dortmund kwa ajili ya saini ya Hummels au kwa PSG kwa ajili ya kumsajili Thiago Silva.
Hivyo United bado wanaweza wakawa na nafasi japo finyu kuweza kumsajili kiungo huyo.