Friday, July 5, 2013

JESHI LA POLISI MKOANI MARA LINAWASAKA WANAWAKE WAWILI KWA KUTUPA VICHANGA

polisi mkoani Mara linawasaka Wanawake wawili ambao wanadaiwa kuwatelekeza kwa kuwatupa watoto wawili wachanga katika matukio mawili tofauti yaliyotokea katika Manispaa ya Musoma.


Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake,Kamanda wa polisi mkoani Mara Ferdinand Mtui alisema jeshi la polisi bado linaendelea kumsaka Mwanamke mmoja ambaye alitelekeza mtoto wake mchanga wa kiume mwenye umri wa siku mbili juni 24 maeneo ya Bweri na kuokotwa na dereva wa bodaboda.

Katika tukio hilo,dereva wa pikipiki huyo aliyetambulika kwa jina la PeterPhinias Mkazi wa Rwamlimi akiwa katika mizunguko yake alimuokota mtoto huyo akiwa ndani ya shimo huku akiwa hai.

Alisema baada ya kumuokota alimpeleka katika kituo cha polisi kati Musoma na muda mfupi baada ya kuokotwa mtoto huyo mama mmoja aitwaye Kulwa Julius alijitokeza na kudai mtoto huyo ni mjukuu wake na kumkabdhi kwa ajili ya matunzo zaidi huku Jeshi la polisi likiendelea kumtafuta Mwanamke aliyetupa mtoto huyo.

Katika tukio lingine,Kamanda Mtui alisema mnamo julai 3 majira ya saa 6 mchana maeneo ya kambi ya polisi (FFU) Musoma aliokotwa mtoto anayesadikiwa kuwa na umri wa mwezi mmoja mwenye jinsia ya kike.

Alisema mtoto huyo alitelekezwa nyuma ya nyumba ya askari polisi na mtu ama watu wasiojulikana na kugunduliwa a wapita njia ambao walitoa taarifa jeshi la polisi na kwenda kumchukua eneo la tukio.

Mtui alisema bada ya mtoto huyo kuchukuliwa alipelekwa kituo cha polisi baadae kupelekwa hospitali ya Serikali ya mkoa wa Mara kwa lengo la kuangaliwa afya yake pamoja na hifadhi.

Kamanda wa polisi mkoani Mara alidai uchunguzi wa kina bado unaendelea kubaini mzazi wa mtoto huyo na kuweza kufikishwa katika vyombo vya seria huku akitoa wito kwa yoyote mwenye taarifa juu ya wazazi hao aweze kuitoa.

Aidha kamanda Mtui alisema jeshi la polisi katika kipindi cha mwezi mmoja kimekamata makosa 120 yakiwemo ya kuvunja nyumba usiku na kuiba,kupatikana na mali inayodaiwa ya wizi,kupatikana na nyara za Serikali,madawa ya kulevya pamoja na wizi wa mifugo.

Alisema makosa hayo yalipatikana baada ya kuendesha msako katika Wilaya ya Musoma,Serengeti,Bunda na Butiama na kufanikiwa kupatikana wahalifu wa makosa mbalimbali wapatao sitini na tatu (63).